Novena:
Siku ya kwanza
TWATEGEMEA SANA
WEMA WA MUNGU
"Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni,
nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;
kwa maana kila aombaye
hupokea, naye atafutaye huona, naye
abishaye atafunguliwa" (Mt 7:7-8).
Baba mwema, Mwenye Heri Yosefu
Allamano alionja maishani mwake upendo
wako wenye huruma na anatuhimiza
kusali kwa imani kubwa, bila kuwa na "hofu ya
kutopata tunaloomba", kwani wewe "yote
huwajalia wanaokuamini". Kwa tumaini
kubwa na moyo wa ki-mwana, tunaukimbilia
wema wako wa kibaba na, kwa
maombezi ya Mtumishi wako mwaminifu,
tunakuomba neema ya...
Kama wana Kanisa, tunakuomba upeleke watenda
kazi wengi katika shamba lako, ili
kueneza Neno la wokovu hadi miisho ya
dunia (rej. Mdo 1:8). Kwa Kristo Bwana
wetu. Amina.
Baba yetu,…
Salamu Maria,…
Atukuzwe,…
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya pili
TUMWAMINI MUNGU
APENDAYE KUTUSAIDIA
"Nanyi mkiwa katika kusali, msipayukepayuke,
kama watu wa mataifa;
maana wao hudhani ya kuwa
watasikiwa kwa sababu ya maneno
yao kuwa mengi. Maana Baba yenu
anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba" (Mt 6:7-8).
Baba yetu, Mwenyeheri Yosefu Allamano
alielewa vizuri juhudi zako kwa wanao
wote, hasa wenye shida, na anatuhakikishia
"kuwa yeyote akuaminiye hatafadhaika kamwe" kwani
"wewe huweza, hujua na hupenda kutusaidia."
Maneno haya yanatutia moyo na
kutuwezesha kukuomba kwa imani kubwa
katika wema wako usio na mwisho.
Kwa maombezi ya Mtumishi wako mwaminifu,
tunakuomba neema ya...
Pamoja na wote wakuaminio, tunakuomba
sana ueneze Ufalme wako wa upendo
na amani ulimwenguni kote (rej. Mt
24:14). Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Baba yetu,…
Salamu Maria,…
Atukuzwe….
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya tatu
MATUMAINI KATIKA
MAJALIWA YA BABA
" Waangalieni ndege wa angani, ya
kwamba hawapandi, wala hawavuni,
wala hawakusanyi ghalani; na Baba
yenu wa mbinguni huwalisha hao.
Ninyí je, si bora kupita hao?" (Mt
6:26).
Baba Mjaliwa, Mwenye Heri Yosefu
Allamano alipata kuona msaada wako siku
zote za maisha yake na anathibitisha
kuwa “tusisite kutumainia majaliwa
yako", kwani "wewe, unayewalisha ndege,
hakika utatujalia na sisi kwa wingi."
Tunakukimbilia wewe uliye karibu nasi
daima na uliye mwangalifu kwa mahitaji
yetu. Kwa maombezi ya Mtumishi wako
mwaminifu, tunakuomba kwa imani ya
ki-mwana neema ya...
Tukiungana na wabatizwa wote, tunaomba
ili Kanisa lako lienee na kukua kati ya
mataifa yote na, kama chachu ilivyo katika
unga, liyabadilishe kwa nguvu ya Injili
(rej. Lk 13:20-21). Kwa Kristo Bwana
wetu. Amina.
Baba yetu,…
Salamu Maria,…
Atukuzwe….
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya nne
TUMWAMINI
MUNGU BILA HOFU
"Mkimwomba Baba neno lolote
atawapa kwa jina langu. Ombeni,
nanyi mtapata, furaha yenu iwe timilifu"
(Yn 16.23-24).
Baba mwaminifu sana kwa kila ahadi,
Mwenyeheri Yosefu Allamano alikuamini daima,
wewe uliye mwangalifu kwa viumbe
vyako, na unatushauri "kuweka yote
mikononi mwako, bila hofu, kwani wewe
huachi kazi zako bila kuzikamilisha," wala
hughairi matumaini wanayokutumainia
wana wako. Tukiwa na hakika hii ya
kwamba daima unasikiliza maombi yetu,
tunajitolea kwako kabisa na, kwa
maombezi ya Mtumishi wako mwaminifu, tunakuomba
neema ya...
Tukiungana na Kanisa la kimisionari ulimwenguni kote,
tunakuomba ili Mwana wako, uliyemtuma
kuuokoa ulimwengu wote (rej. Yn 3:17),
ajulikane na watu wote kama Mchungaji
Mwema na hatimaye duniani pawepo
na kundi moja na mchungaji mmoja
(rej. Yn 10:16). Kwa Kristo Bwana wetu.
Amina.
Baba yetu,… Salamu Maria,… Atukuzwe,...
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya tano
NILIMTUMAINIA MUNGU
"Je, mashomoro watano hawauzwi
kwa senti mbili? Wala hasahauliwi
hata mmojawapo mbele za Mungu.
Lakini hata nywele za vichwa vyenu
zimehesabiwa zote. Msiogope basi,
bora ninyi kuliko mashomoro wengi"
(Lk 12:6-7).
Baba Mwenyezi wa huruma, Mwenye
Heri Yosefu Allamano hakukosa kutumainia
msaada wako katika kila hitaji, na
anatufundisha "kuendelea kuuamini upendo
wako bila kukata tamaa, hata tusipopata
yote", ama "inapotubidi kusubiri, ili
kutujaribu na kutukumbusha kuwa sisi ni
maskini."
Kwa dhana hii moyoni, tunadhihirisha
imani yetu ya siku zote katika
moyo wako wa Baba na, kwa maombezi
ya Mtumishi wako mwaminifu, tunakuomba
neema ya...
Kwa ajili ya wale wasiokufahamu bado,
tunakuomba uwasindikize watangazaji wa
Injili, ili jina lako takatifu lijulikane na
kusifiwa duniani kote (rej. Mdo 2:21).
Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Baba yetu,…
Salamu Maria,…
Atukuzwe,…
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya sita
TWASADIKI WEMA WA
BWANA
"Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua
kuwapa watoto wenu vipawa vyema,
je, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni
atawapa mema wao wamwombao?"
(Mt 7:11).
Baba mwema, Mwenyeheri Yosefu
Allamano alithibitisha kuwa ukarimu
wako hauna kifani, na anatuhakikishia
kuwa "wewe ungependa sisi tuwe na
imani katika wema wako", tuweze "kuja
kwako hata katika jambo dogo na kukutumainia
wewe peke yako, bila kujali
matukio yajayo". Tukiamini ukarimu
wako, tunakujia wewe uliye mwema sana
na, kwa maombezi ya Mtumishi wako
mwaminifu, tunakuomba neema ya...
Kwa kufuata mfano wa Mwana wako
ambaye, ingawa alikuwa Mungu,
alijifanya kuwa hana utukufu,
akatwaa hali ya mtumwa, akawa mtii
hata mauti ya msalaba (rej. Flp 2:7-8),
Kanisa lijue kujishughulikia zaidi na zaidi
kwa ajili ya wanaoteseka kwa sababu ya
umaskini, vita na ukosefu wa kila aina wa
haki. Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Baba yetu,… Salamu Maria,… Atukuzwe,...
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya saba
UJASIRI WA KUSALI
WATOKANA NA IMANI
"Mkiwa na imani, msipokuwa na
shaka, hata mkiuambia mlima huu:
Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka.
Na yoyote mtakayoyaomba katika
sala mkiamini, mtapokea." (Mt 21:21-
22).
Baba, upokeaye maombi ya wanao,
Mwenyeheri Yosefu Allamano, ili apate
msaada kwako, alionesha daima ustahimilivu
mkubwa na anatufundisha kuwa "ili
tupate neema tunapaswa kuiomba kwa
imani kubwa, kwa ujasiri ule wa kuweza
kutenda miujiza," na kututia moyo kwa
maneno haya: "Jipeni moyo kila
wakati na tusonge mbele katika Bwana."
Tukijipa moyo kwa mafundisho yake,
tunakujia wewe unayetutunza kwa upendo
na, kwa maombezi ya Mtumishi wako
mwaminifu, tunakuomba neema ya...
Tukiungana na watu wote wenye mapenzi
mema, tunakusihi toka mawio ya jua hata
machweo yake uwakusanye watoto wako
wote waliotawanyika na uwakaribishe katika
karamu ya Ufalme wako (rej. Mt 8:11).
Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Baba yetu,… Salamu Maria,… Atukuzwe,...
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya nane
TUENDELEE KUTARAJIA
YASIYOWEZA KUTARAJIWA
"Msisumbuke, basi, mkisema: Tule
nini? au Tunywe nini? au Tuvae nini?
Kwa sababu Baba yenu wa mbinguni
anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
Basi msisumbuke ya kesho" (Mt 6:31-
34).
Baba, unayetoa tunu za kustaajabisha,
Mwenyeheri Yosefu Allamano, Nata katika
nyakati zilizo ngumu katika maisha, alitarajia
yasiyoweza kutarajiwa (rej. Rum
4:18) na anatuonya "tuwe na tumaini lililo
hai moyoni, tuwe na tumaini kubwa
kabisa, kwani anayetumaini kidogo tu
anakukosea wewe", uliye na wema bila
mipaka. Tukifuata mfano wake mzuri,
tunapenda kukuonesha tumaini letu
kubwa katika ukarimu wako wa kibaba na,
kwa maombezi ya Mtumishi wako
mwaminifu, tunakuomba neema ya...
Tukiamini ya kuwa unataka "watu wote
waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli"
(1Tim 2:4), tunakusihi sana utume mwanga
wa Roho wako, ili "kila ulimi ukiri ya
kuwa Yesu Kristo ni Bwana" (Fip 2: I 1).
Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Baba yetu,… Salamu Maria,… Atukuzwe,...
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Siku ya tisa
MAPENZI MATAKATIFU
YA MUNGU YAFANYIKE
"Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini
mimi nitawaona tena, na mioyo
yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna
awaondoleaye. Tena siku ile hamtaniuliza
neno lolote" (Yn 16:22-23).
Baba, Mungu wetu, Mwenyeheri Yosefu
Allamano, akifuata mfano wa Mwana
wako mpendwa, alitenda daima yaliyokupendeza
(rej. Yn 8:29) na anatufundisha ya
kuwa "upo katika yote, hata yaliyo madogo
na kuyatawala kwa manufaa yetu, ukituomba
kutii kwa moyo amri zako za upendo".
Tukithibitisha utayari wetu wa kutimiza
kwa moyo mapenzi yako matakatifu, yoyote
yale yatakayokuwa, hatusiti kuendelea
kukuomba, kwa tumaini lile lile, kutujalia
kwa upendo neema ya...
Kwa nguvu ya imani yetu ya kikristo,
tunakuomba sana ili familia nzima ya mwanadamu
iweze kumtambua Kristo kama
Mwokozi wa pekee wa ulimwengu, yeye
anayeishi na kutawala nawe, katika umoja
wa Roho Mtakatifu, daima na milele (rej.
Yn 4:42). Amina.
Baba yetu,… Salamu Maria,… Atukuzwe,...
Bikira Maria Consolata, utuombee.
Sala ya mwisho
SHUKRANI
Ee Baba, chemchemi ya kila kilicho
chema, wimbo wetu wa sifa upae kwako
kwa ajili ya mapaji uliyomjalia Mwenye
Heri Yosefu Allamano.
Katika Kanisa lako alikuwa kuhani wa
agano jipya, mhudumu wa faraja, mshauri
mwenye busara na hekima, mwenye
kutafuta daima mapenzi yako.
Baba Allamano, mwenye bidii kwa ujio
wa ufalme wako, akawa Baba na Kiongozi
wa Familia za Watawa Wamisionari
pamoja na Maria, mmisionari wa kwanza
wa Injili, wamtangaze duniani kote Kristo
Mkombozi.
Ee Mungu Baba, utujalie kuiga mfano
wake na kushiriki katika kazi ya
Ukombozi, ili watu wote wawe na uzima,
kisha wawe nao tele.
Kwa Kristo Bwana wetu. Amina